Na Clezencia Tryphone
BAADA ya uvumi wa muda mrefu kuhusu usajili wa kiungo, Amri Kiemba, hatimaye uongozi wa Simba, umefanikiwa kumbakiza Msimbazi kwa miaka mwili ijayo.
Kiungo huyo ambaye yuko kwenye kiwango kizuri hivi sasa, habari zilizagaa kuwa mahasimu wa Simba, Yanga nao walikuwa kwenye harakati za kusaka saini yake kwa ahadi ya kitita cha sh milioni 30, jambo lililowalazimu Simba kuongeza hadi milioni 35 na kufanikiwa kumbakiza.
Kwa mujibu wa wakala wa Kiemba, Ulimwengu Hamim, kiungo huyo alisaini mkataba wa miaka miwili kuendelea kuichezea Simba jana mchana.
Habari za Kiemba ambaye pia anakipiga timu ya taifa ‘Taifa Stars’ kurejea Yanga alikowahi kuitumikia miaka ya nyuma, ziliibua mjadala na kuwaweka katika wakati mgumu mashabiki wa Simba, ambao bado wana kumbukumbu nyota mwingine, Mrisho Ngasa, ambaye alikipiga Msimbazi nusu msimu na hatimaye kurejea Jangwani.
Awali, Kiemba alidai kuwa soka ndiyo ajira yake hivyo kupitia kwa wakala wake, angeangalia pa kwenda patakapomridhisha.
Kiemba hivi sasa yuko kwenye midomo ya wapenzi na mashabiki wa soka, hasa baada ya mwishoni mwa wiki kuonyesha kiwango cha juu katika mechi ya kuwania kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia, kati ya Stars na Morocco, ambako bao lake liliacha gumzo. Katika mechi hiyo, Stars ililala 2-1 ugenini.
Katika hatua nyingine, kocha mkuu wa Simba, Abdallah Kibadeni, amesema licha ya kuumia kwa beki wao wa kimataifa, Samuel Senkoomi, raia wa Uganda, wanamsubiri aweze kupona ili aendelee kumchunguza ili kuona kama anawafaa katika kikosi chao.
Senkoomi beki aliyetua Msimbazi akitokea URA, aliumia kifundo cha mguu katika mazoezi ya timu hiyo kwenye Uwanja wa Kinesi jijini Dar es Saalam.
Kibadeni, akizungumza mara baada ya kumaliza mazoezi kwenye uwanja huo, alisema, wanatarajia kumtumia mchezaji huyo, ila mpaka kiwango chake kimvutie ili aweze kusajiliwa.
“Nimemtazama, ila bado sijamtazama vizuri, kwa kuwa siku mbili tu za mazoezi akaumia, nasubiri aweze kupona halafu nimwangalie kama atatufaa,” alisema Kibadeni. Aidha alisema anatarajia kupata kikosi cha kwanza wiki ijayo, baada ya nyota walioko timu ya taifa kuungana na wenzao.
“Ningeishapata kikosi, ila nawangoja vijana waliokuwa timu ya taifa, nina imani wakija nitapata kikosi cha kwanza,” alisema. Kibadeni, nyota wa zamani wa Simba, Majimaji na Taifa Stars, amerejea Msimbazi kuchukua mikoba ya Mfaransa, Patric Liewig, ambaye katupiwa virago kutokana na matokeo mabovu, akitokea Kagera Sugar.
No comments:
Post a Comment