Front page

MATANGAZO

KARIBU

Thursday, July 4, 2013

RT: Vijana waliong’ara Arusha waendelezwe

Mwalimu Samwel Tupa  akifuatilia kwa makini moja ya michezo mkoani Arusha...Mwalimu huyu ndiye aliyekuwa na jukumu la kuwanoa vijana walioshindana katika mashindano ya riadha hivi karibuni.Mashindano hayo yameshirikisha nchi za Afrika Mashariki na Kati.

Na Hosea Joseph

SHIRIKISHO la Riadha Tanzania (RT), limewataka wadau na wapenzi wa riadha nchini, wawaunge mkono wanariadha waliong’ara kwenye mashindano ya Kanda ya Afrika Mashariki na Kati kwa vijana chini ya miaka 20 yaliyomalizika hivi karibuni jijini Arusha ili kujenga timu bora ya taifa ya baadaye.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Katibu Mkuu wa RT, Mujaya Suleiman Nyambui, alisema, vijana waliopatikana kwenye mashindano ya shule za sekondari (Umisseta), wameonesha uwezo mkubwa katika mashindano hayo, hivyo kubeba matumaini ya siku zijazo katika mashindano ya kimataifa, ambako wanahitaji kuwezeshwa ili wasonge mbele.

Alisema, kutokana na uwezo wa juu waliouonesha vijana hao katika michezo ya kurusha mkuki na kisahani, ambako walifanikiwa kuzoa medali za dhahabu na fedha, ni fursa kwa Tanzania kuwashika mkono ili wasivunjike moyo na kuacha mazoezi.

“Tunahitaji timu bora ambayo inaweza kutuwezesha kufikia mafanikio, lakini hatuna fedha za kuwaendeleza wachezaji, lakini kama jamii itawaunga mkono vijana walioshiriki mashindano Arusha tunaweza kupata timu nzuri baadaye,” alisema Nyambui.

Nyambui alisema, wao kama Shirikisho, waliamua kutumia wachezaji kutoka shule za sekondari ili kuanza upya mkakati wa kuandaa vijana wapya watakaofufua mchezo wa riadha hapa nchini, ambao ulikuwa tegemeo kwa nchi kimataifa miaka ya 70 na 80.

No comments:

Post a Comment