Front page

MATANGAZO

KARIBU

Saturday, April 13, 2013

UN kutuma wanajeshi 3,069 mashariki mwa Kongo

Saturday, 13 April 2013 19:40

UN kutuma wanajeshi 3,069 mashariki mwa Kongo

Umoja wa Mataifa umetangaza kuwa, utatuma kikosi cha askari 3,069 mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa shabaha ya kwenda kupambana na makundi ya waasi katika eneo hilo. 

Madnodje Mounoubai, Msemaji wa vikosi vya kusimamia amani vya Umoja wa Mataifa huko Kongo DRC ametangaza kuwa, idadi hiyo ni rasmi na kwamba, askari hao wataungana na vikosi vingine vya umoja huo vilivyoko Kongo. 

Afrika Kusini, Tanzania na Malawi zimetajwa kuwa ndizo zitakazounda kikosi hicho cha kimataifa. Hata hivyo hivi karibuni Afrika Kusini ilisema kuwa haina mpango wa kutuma majeshi yake mashariki mwa Kongo. Msemaji wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kikosi hicho cha kimataifa kitaongozwa na jenerali kutoka Tanzania ambaye hakumtaja jina lake. 

Hatua ya kutumwa kikosi cha Umoja wa Mataifa mashariki mwa Kongo ni kutekeleza azimio la Baraza la Usalama la mwezi Machi uliopita ambalo linataka kupelekwa kikosi cha kimataifa katika maeneo ya mashariki mwa nchi hiyo ili kupambana na makundi ya waasi. Wakati huo huo, waasi wa M23 wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameionya serikali ya Tanzania na kuitaka iachane na uamuzi wake wa kutaka kutuma majeshi yake Kongo DRC.

source.....idhaa ya Tehran

No comments:

Post a Comment