Front page

MATANGAZO

KARIBU

Saturday, January 11, 2014

Kuanza kampeni za uchaguzi nchini Afrika Kusini

Rais Jacob Zuma wa Afrika Kusini jana Ijumaa alifungua rasmi kampeni za uchaguzi mkuu wa nchi hiyo akiwataka wananchi wakipe kura zao chama tawala cha ANC. Leo Jumamosi tarehe 11 Januari, Rais huyo wa Afrika Kusini anatarajiwa kutoa hotuba yake ya kwanza ya kampeni za uchaguzi katika eneo la Mbombela la mashariki mwa nchi hiyo na kutangaza ilani na sera za chama
chake cha ANC.
Wachambuzi wa masuala ya kisiasa wanaamini kuwa, mkutano wa leo wa hadhara uliopangwa kuhutubiwa na Rais Jacob Zuma, utakuwa ni mtihani mzuri wa kuangalia chama cha ANC chini ya uongozi wa Zuma, kina umaarufu kiasi gani huko Afrika Kusini. Mwaka 2009 Zuma alichaguliwa kuwa Rais wa Afrika Kusini na mwenyekiti taifa wa chama cha ANC. Hata hivyo umaarufu wa Zuma umepungua sana katika miezi ya hivi karibuni kutokana na masuala tofauti. 

Tuhuma mbalimbali za ubadhirifu unaodaiwa kufanywa na Zuma na wasaidizi wake na kuweko kiwango kikubwa cha umasikini, ukosefu wa kazi na vitendo vya uhalifu nchini Afrika Kusini, ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuwa yamechangia kupunguza umaarufu wa Rais Jackob Zuma. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, hata kama chama cha ANC kimeweza kulinda umaarufu wake mbele ya wananchi, lakini mapenzi kwa Jacob Zuma kama Zuma yamepungua mno na si jambo lililo mbali kuona baadhi ya wafuasi wa chama hicho wakihamia kwenye vyama vingine kutokana na kuchukizwa kwao na Jacob Zuma.

Hii ni katika hali ambayo kushindwa chama cha ANC kutimiza ahadi zake pamoja na kashfa za ubadhirifu wa fedha unaodaiwa kufanywa na Rais Jacob Zuba kumevifanya baadhi ya vyama vya Afrika Kusini vitoe mwito wa kupokonywa madaraka chama cha ANC. Vyama vya upinzani nchini humo vinamuhesabu Zuma kuwa ndiye chanzo cha kudhofika idara ya mahakama ya nchi hiyo, kuongezeka ukosefu wa kazi na kupungua daraja ya itibari ya Afrika Kusini. Katika miezi ya hivi karibuni nchi hiyo imeshuhudia migomo ya mfululizo jambo ambalo limepelekea kupungua vibaya daraja ya kiuchumi ya Afrika Kusini. 

Wapinzani wa Zuma wanaona kuwa, elimu nayo imeingia katika mgogoro kutokana na siasa za serikali ya Zuma. Weledi wa mambo wanaamini kwamba, kama migogoro itaendelea huko Afrika Kusini, basi kuna uwezekano wa kutokea mabadiliko makubwa ya kisiasa nchini humo na kuathiri ushindi wa chama tawala katika uchaguzi ujao. Hasa kwa kutilia maanani kuwa, vyama vingine vinanufaika na kupungua umaarufu wa chama tawala cha ANC na vinajipanga kutumia fursa hiyo kujinyakulia kura nyingi zaidi na kushinda katika uchaguzi ujao....IDHAA YA TEHRAN

No comments:

Post a Comment