Baada ya uchaguzi mkuu kufanyika Zimbabwe, sasa nchi hiyo inaonekana kuelekea katika mzozo wa kisiasa kwa sababu ya matokeo ambayo bado si rasmi. Mgombea wa urais Morgan Tsvangirai anadai kuwa uchaguzi haukuwa halali.
Matokeo rasmi ya uchaguzi mkuu wa Zimbabwe bado hayajatolewa lakini Rais Robert Mugabe anaamini kwamba ataibuka mshindi. "Inatarajiwa kwamba rais Mugabe atashinda kwa asilimia 70 mpaka 75," alisema Rugare Gumbo, msemaji wa chama tawala cha ZANU-PF.
Waangalizi wa Umoja wa Afrika wamesema Ijumaa kuwa kwa mtazamo wao uchaguzi wa Zimbabwe ulikuwa wa kuaminika na wa haki. Hata hivyo waangalizi hao wamekiri kwamba pamekuwa na hitilafu katika daftari la wapiga kura na baadhi ya wapiga kura ambao hawakuruhusiwa kuingia katika vituo vya uchaguzi.
Waziri Mkuu Morgan Tsvangirai ambaye ni mpinzani wa karibu zaidi wa Mugabe, amekosoa hitilafu hizo vikali na kusema kwamba uchaguzi si halali wala wa haki. "Haimaanishi kwamba SADC na Umoja wa Afrika ndio vigezo vya kimataifa vya uchaguzi wa huru na wa haki," alisema Tsvangirai.
No comments:
Post a Comment