Watu wasiopungua 15 wakiwemo wanafunzi wa shule wamepoteza maisha huko Kenya baada ya basi walimokuwa wakisafiria kupinduka Jumatano jioni katika kaunti ya Kisii, magharibi mwa nchi hiyo.
Afisa mkuu wa polisi katika eneo la Gucha, Mark Ondego amesema walioshuhudia wanasema basi hilo lilipoteza mwelekeo na kupinduka mara kadhaa. Kati ya miili iliyopatikana ni ya dereva wa basi, wanafunzi na waalimu ambao walikuwa wakielekea katika eneo la Nyamache kwa ajili ya michezo ya shule.
Wakati huo huo Rais Uhuru Kenyatta ametuma salamu za rambi rambi kufuatia ajali hiyo na kuelezea wasiwasi wake kuhusu kuongezeka ajali za barabarani nchini Kenya. Amewataka polisi kuchukua hatua madhubuti za kuhakikisha sheria za barabarani zinatekelezwa.
Aidha Rais Kenyatta ameamuru wale wote waliojeruhiwa katika ajali hiyo wasafirishwe kwa ndege kutoka Kisii hadi Nairobi kwa ajili ya matibabu katika Hospitali ya Taifa ya Kenyatta.
No comments:
Post a Comment