Friday, July 12, 2013
Shirika la Msamaha Duniani laionya Zimbabwe
Shirika la Kimataifa la Msamaha Duniani Amnesty International, limevionya vikosi vya usalama nchini Zimbabwe, kutokana na ukandamizaji dhidi ya wanaharakati wa haki za binaadamu na wapinzani wa serikali nchini humo.
Mratibu wa mipango ya shirika hilo barani Afrika Bwana Noel Kututwa amesema kuwa, hatua zinazochukuliwa na vikosi vya usalama vya Zimbabwe zinatia wasiwasi mkubwa kuhusu hatari ya kufanyika uchaguzi mkuu katika hali ya ukandamizaji mkubwa dhidi ya wanaharakati wa haki za binaadamu na wapinzani wa serikali ya Zimbabwe.
Kututwa amewataka askari usalama nchini humo kuheshimu haki ya kujieleza. Uchaguzi mkuu nchini Zimbabwe unatazamiwa kufanyika tarehe 31 mwezi huu. Katika ripoti yake ya kurasa 63, Amnesty International yenye makao yake mjini London, Uingereza, ilitangaza kuwa, pamoja na kupungua vitendo vya ukandamizaji wa polisi nchini Zimbabwe ikilinganishwa na wakati wa uchaguzi uliopita, lakini bado wanaharakati wa haki za binaadamu na wapinzani nchini humo wanasumbuliwa na hali mbaya ya ukandamizaji.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment