Umoja wa Mataifa wakataa ombi la Kenya kuhusu ICC |
Ombi hilo la Kenya kwa mara nyingine limepingwa vikali na mataifa ya magharibi katika baraza hilo la usalama lenye wanachama 15 na kuwaambia viongozi hao wa Kenya katika kikao cha faragha kuwa sharti wakabiliwe na mashitaka hayo katika mahakama ya ICC.
Balozi wa Kenya katika Umoja wa Mataifa, Macharia Kamau, baada ya mkutano huo wa faragha amesema Kenya imetaka kesi hizo kusitishwa haraka iwezekanavyo na kuongeza kuwa jinsi zitakavyositishwa na nani atakayezitisha hilo ni suala jingine lakini bila shaka zinahitaji kutupiliwa mbali kwani zinatatiza amani na haki nchini Kenya.
Rais Uhuru Kenyatta, naibu wa Rais William Ruto na mtangazaji Joshua arap Sang wanakabiliwa na mashitaka ya uhalifu dhidi ya binadamu kwa madai ya kuhusika katika ghasia za baada ya uchaguzi mkuu mwaka 2007 ambazo zaidi ya watu 1,000 waliuawa. Wote watatu wamekanusha madai hayo.
Rais wa Kenya Uhuru na naibu wake Ruto
Kesi dhidi ya Kenyatta imepangiwa kuanza mwezi Julai mwaka huu na ameahidi kushirikiana na mahakama ya ICC, lakini wakati huo huo akifanya kampeini kabambe dhidi ya kesi hiyo.
Kulingana na hati za Umoja wa Afrika, Kenya inazirai nchi nyingine barani Afrika kuishawishi mahakama ya ICC kutupilia mbali kesi dhdi ya viongozi hao. Nchi nyingi za Afrika ni wanachama wa mkataba wa Roma uliobuni mahakama hiyo ya kimataifa, lakini kumekuwa na mashaka miongoni mwa mataifa hayo kuwa ICC inawalenga viongozi wa Afrika pekee katika kesi zake.
No comments:
Post a Comment