MWAKILISHI wa Papa Francisco hapa nchini,Balozi Francisco Padilla amenusulika kuuawa kwa bomu  baada ya mtu asiyejulikana  kurusha bomu la mkono katikati ya waumini na kujeruhi watu 30 ,wakati akisoma misa ya uzinduzi wa kanisa katoliki la mtakatifu Joseph mfanyakazi,
nje kidogo ya jiji la Arusha.

Aidha Kanisa hilo,askofu mkuu wa kanisa katoliki jimbo kuu la Arusha,Josephat Lebulu pamoja na  mabadri zaidi ya 200 waliokuwepo kwenye misa hiyo walinusulika  kulipukiwa kwa bomu linalodaiwa kutekelezwa na vikundi vya kigaidi vilivyoanza kujipenyeza hapa nchini
.

Hali hiyo ilizua taharuki  kwa waumini walikuwa zaidi ya 1000 waliokuwa wamefurika eneo la tukio huku vilio vikisikika na watu kukumbia ovyo na wengine kulaliana wakijaribu kuokoa maisha yao.

Tukio hilo limetokea leo majira ya saa 4.30 asubuhi wakati Askofu Lebulu na mwalikishi wa papa wakibariki maji nje ya kanisa hilo kabla ya kukata utepe kama ishara ya uzinduzi wa kanisa hilo jipya
lililojengwa kwa nguvu ya waumini eneo la Olasiti .

Waliojeruhiwa katika tukio hilo wengi wao walionekana kuvuja damu nyingi baada ya kukatika viungo na wengine kuonekana wakiwa wamechanwa chanwa hali iliyolazimu magari mbalimbali yakiwemo ya kuokoa kwenye majanga yalifika na kuwakimbiza hospitali.

Kabla ya tukio hilo waumini wa kanisa hilo walifanya maandamano kuanzia kanisa katoliki la Burka ambalo ni kanisa mama wakiongozwa na askofu mkuu, Lebulu na ilipofika majira ya saa 3.30 walifika katika kanisani hilo la mtakatifu Joseph.

Muda mfupi msafara wa balozi wa Vatcan,hapa nchini  ulifika na kiongozi huyo kulakiwa na mwenyeji wake ambaye ni askofu Lebulu na kisha kumtembelea kanisa hilo jipya  kabla ya kukata utepe ambapo tukio hilo lilikuwa lifanyike kabla ya kuanza misa takatifu.

Aidha baada ya kutembelea kanisa hilo,lilifuata tendo la kubariki maji ili yapatikane maji  ili maji hayo yatumike kubariki kanisa hilo ikiwemo kuyachanganya na chumvi ,ambapo wakati tendo hilo likiendelea ndipo mlipuko mkubwa ulioambatana na vilio ulisikika na kusababisha
tahariki kubwa kwa waumini na watu mbalimbali waliopo eneo hilo.

Akizungumza na gazeti hili mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo ambaye hakutaka kutaja jina lake,alisema kuwa wakati misa ikiendelea alimwona mtu mmoja mwanaume akiwa amevaa koti la mvua na kujifunika na kofia kichwani  ambapo alitokea upande wa kushoto mwa kanisa hilo na kutupa kitu kilichotoa mlipuko.

‘’mimi nilikuwa nimesimama gorofani nikamwona mtu akiwa na koti la mvua akisogea mbele ya kanisa na kurusha kitu kilichotoa mlio mkubwa na baadae watu walianza kulia kwa sauti ndio nikajua lilikuwa ni bomu.

Kamanda wa polisi mkoa wa Arusha,Liberatus Sabas  pamoja na maafisa mbalimbali wa polisi na viongozi viongozi wa serikali na vyama vya siasa walifika katika eneo la tukio ambapo umati mkubwa wa watu ulikusanyika huku kukutawaliwa na vilio na majonzi kwa baadhi ya ndugu
na jamaa ambao walikuwa hawaoni ndugu zao.

Naye mkuu wa mkoa wa Arusha,Magesa Mulongo aliwataka wanachi kuwa watulivu wakati vyombo vya dola wakiendelea na uchunguzi wa tukio hilo hata hivyo alisema kuwa polisi kutoka makao makuu ya jeshi pamoja na wataalamu wa mabomu kutoka makao makuu wanatarajiwa kufika katika eneo la tukio ili kuongeza nguvu katika kubaini tukio hilo.

Aidha alisema kuwa jumla ya majeruhi  zaidi ya 30 wakiwemo watatu wenye hali mbaya wamelazwa katika hospitali ya mkoa Mount Meru kwa ajili ya matibabu.

Hata hivyo kumekuwepo na taarifa ya kushikiliwa kwa mtu mmoja akihusishwa na tukio hilo japo kamanda wa polisi mkoa wa Arusha alisema atatoa ufafanuzi hapo baadae.