Wednesday, May 22, 2013
Fisi avuruga kijiji, ajeruhi wawili
Na Joseph Malembeka, Kongwa
WATU wawili wa kijiji cha Ngomani, wilayani Kongwa mkoani Dodoma wamenusurika kufa baada ya kuvamiwa na fisi ndani ya nyumba yao na kuwajeruhi sehemu mbalimbali za miili yao.
Mbali na watu hao pia mifugo ikiwemo mbuzi na kuku imeuawa na mingine kujeruhiwa kutokana na shambulio hilo.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti kijijini hapo, mashuhuda wa tukio hilo akiwemo Renald Mbogolo na Mwanaisha Hamadi walisema tukio hilo lilitokekea Mei 20, mwaka huu, majira ya saa moja asubuhi.
Waliojeruhiwa katika shambulio hilo ni Mohamed Mwisongo (25) na Ndaiga Simawanga (27) ambao wamelazwa katika hospitali ya wilaya ya Kongwa kwa ajili ya matibabu.
“Mwisongo amejeruhiwa mkono wa kushoto na kifuani na Simanga ameliwa tako la kushoto na wamekimbizwa hospitalini kwa matibabu,” alisema Mbogolo.
Akitoa ufafanuzi wa tukio hilo, mwenyekiti wa kijiji hicho, Emanuel Lusito, alisema tukio hilo lilianza kwa Simanga asubuhi muda mfupi baada ya kuamka na kwenda nje kujisaidia.
Alisema aliporudi ndani kulala, akiwa kitandani bila kufunga mlango kwa komeo kwa vile kulishakuchwa, fisi huyo aliingia hadi chumbani na kuanza kumnyofoa sehemu ya makalio jambo lililosababishia apige kelele.
Alisema kutokana na kelele hizo, Mwisongo alikimbilia chumbani kwa Simanga akitaka kumsaidia, lakini ghafla fisi huyo alimgeukia na kuanza kumrarua maeneo ya mkono wa kushoto na kifuani.
“Tukio hili la fisi kutokea limesabababisha taharuki kubwa..., na fisi huyo amekatwa kichwa ambacho tunataka tukipeleke maabala mkoani Dodoma kwa ajili ya uchunguzi ili kubaini kama alikuwa na ugonjwa, tuudhibiti,” alisema Lusito.
“Mbali na zoezi hili tumeshatoa taarifa kituo cha polisi Kibaigwa na tunataraji kufikisha suala hili idara ya wanyamapori ili watusaidie kukabiliana na wanyama pori ambao wamekuwa wakijitokeza hasa kipindi hiki cha mavuno,” alisisitiza Lusito
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment