Mganga Mkuu Mfawidhi wa Hospitali ya Songea, Dk. Benedict Ngaiza, amesema kuwa watoto wote watano wamefariki muda mfupi tu kwa vile mapafu yao ni madogo sana na hayana uwezo wa kuvuta hewa.
Dk Ngaiza ameyasema hayo leo hii wakati akizungumza na JAMBO FESTIVAL OFFICIAL BLOG kuhusiana na tukio hilo la aina yake.
Hapo jana MWANAMKE mmoja mkazi wa maeneo ya Ruhuwiko katika Halmashauri ya Manispaa ya Songea mkoani Ruvuma, Sophia alijifungua watoto watano.
Dk. Ngaiza alisema wauguzi wa hospitali hiyo walimpa huduma nzuri mwanamke huyo jambo lililosaidia kujifungua salama watoto hao licha ya kufanyiwa upasuaji.
Aliongeza kuwa Sophia alijifungua watoto hao jana majira ya saa 4 asubuhi katika hospitali hiyo huku mtoto wa kwanza akiwa na uzito wa gramu 730, wa pili 810, wa tatu 670, wa nne 820 na wa tano gramu 430.
Alifafanua kuwa kati ya watoto hao waliozaliwa, watatu ni wa kiume na wawili ni wa kike na kudai kwamba tukio hilo ni la kwanza kutokea katika hospitali hiyo ambapo mzao huo ni wa pili kwa mama huyo.
Alibanisha kuwa katika mzao wa kwanza wa mama huyo alijifungua mtoto mmoja.
No comments:
Post a Comment